Wednesday, August 1, 2012

Usiwe zoba, usanii wa wanawake kwenye mapenzi uko hivi!


ASSALAM alaikum mpenzi msomaji wa safu hii maridhawa ya mashamsham. Ni wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii ambayo pamoja na mambo mengine tunazungumzia mada mbalimbali zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Nalazimika kufanya hivi kutokana na ukweli kwamba, mapenzi yanachukua sehemu kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Mapenzi huweza kumfanya mtu akaishi maisha ya raha mustarehe hasa pale anapompata mtu mwenye penzi la kweli lakini pia usipoyajulia yanaweza kukutoa roho.
Mpenzi msomaji wangu, mapenzi yanaweza kumfanya mtu yeyote akachanganyikiwa, awe mwanaume au mwanamke hasa pale ambapo atajitahidi kuonesha mapenzi yake yote lakini mwisho wake akateswa.
Utafiti unaonesha kuwa, wanawake wanaongoza kwa kutoa machozi kisa kikiwa ni kutendwa na wanaume lakini itakuwa ni jambo la aibu kama mwanaume atajitokeza mbele za wenzake na kuanza kutoa machozi kisa kikiwa ni mpenzi wake.
Wiki hii naomba nizungumzie swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza bila kupata majibu sahihi kiasi cha kuwafanya washindwe kuishi maisha ya furaha na wapenzi wao.
Wapo wanaume wengi ambao leo hii wana wapenzi lakini hawaamini kama kweli wanapendwa. Wengi wanahisi kuibiwa tu kutokana na usanii uliotawala.
Huenda hata wewe unayesoma hapa upo kwenye uhusiano lakini humuamini sana mpenzi wako. Kiukweli hakuna ambaye anaweza kujiaminisha kuwa anapendwa na hasalitiwi kwa asilimia zote.
Labda niseme tu kwamba, mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu sana. Unaweza ukajikuta uko na mpenzi ambaye anaonesha kukupenda, kukujali, kukuheshimu sana na kukuita majina kama vile Sweetie, honey, laazizi, mpenzi na mengineyo kiasi cha kukufanya ujihisi mwenye bahati ya kupendwa lakini kumbe hakuna lolote, wizi mtupu.
Leo hii wapo wanawake ambao wanafikia hatua ya kutangaza kwa marafiki zao kuwa, wanaume walionao wanawachuna tu na wala hawana mapenzi ya dhati kwao. Hivi wewe mwanaume unaposikia mwanaume mwenzako anasemwa hivyo unajisikiaje? Unawezaje kuamini kuwa huyo wako uliyenaye hawatangazii wenzake hivyo hivyo?
Ndugu zangu hasa wanaume, unapotokea kumpenda msichana flani unatakiwa kuwa makini sana, ni wachache sana ambao wanaweza kukupa uhakika wa asilimia 100 kuwa wako na wewe tu.
Kuna wasichana ambao leo hii unajua wameolewa lakini wana vibuzi vyao nje. Wapo ambao unajua kabisa wana wapenzi wao lakini unawaona wakijivinjari na wanaume wengine wa pembeni, wewe mwanaume unajisikiaje? Unadhani kuna furaha ya mapenzi kama usanii huu unachukua nafasi kwa wapenzi wetu wengi?
Ndiyo maana sasa hivi wanaume wengi wajanja wanapuuzia mengi na hata wanapoingia kwenye penzi hawaingii kwa miguu miwili. Jaribu kuchunguza utabaini kwamba, wanaume wengi wako mguu nje, mguu ndani. Wanajua siku yoyote penzi litaingia shubiri. Ndiyo ukweli wenyewe ndugu zangu.
Jaribu kuangalia idadi ya mafumanizi, jaribu kuangalia idadi ya watu wanaoachana kwa siku, hakika idadi ni kubwa! Ndiyo maana nasema, kupenda ni haki ya kila mmoja wetu lakini tunapoingia kwenye ulingo huo, tuwe tayari pia kuwakosa hao tuliowapenda na pia tusipende kwa asilimia zote ili kutojipa vidonda vya tumbo.
Laghai wa mapenzi hajifichi
Kuna baadhi ya wanaume naweza kusema ni malimbukeni au mazoba wa mapenzi. Yaani unakuta dume zima linamzimikia demu kiasi cha kuamini kwamba bila yeye maisha yake hayawezi kukamilika.
Hukatazwi kumpenda mtu lakini bahati mbaya inakuwa pale utakapotokea kumpenda mtu asiyekupenda na akajilazimisha kukupenda ili kukuridhisha (anakuuzia mbuzi kwenye gunia).
Walio katika aina hii ya mapenzi wako wengi. Mtu anaona kabisa mwanamke anamsaliti kwa kuwa na uhusiano na wanaume wengine, anakuta sms za mapenzi kutoka kwa wanaume wengine, haheshimiwi wala kuonesha yale mapenzi ya kweli halafu bado anang’ang’ania kumpenda, huo si uzoba jamani?
Ifike wakati basi ukae chini na utafakari penzi analokupa mpenzi wako na kuchukua uamuzi sahihi, kumuacha au kuendelea naye. Usikubali hata siku moja kupotezewa wakati na mtu asiyelithamini penzi lako wakati unajua kabisa ukimuacha huyo unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kumpata mwingine atakayekupenda kwa dhati.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali.

No comments:

Post a Comment