Emmanuel Okwi.
Na Saleh AllySIMBA imepewa taarifa kwamba hadi sasa kiungo wake, Emmanuel Okwi ana asilimia karibia 90 za kufuzu majaribio ya kuichezea FC Red Bull Salzburg ya Austria.
Hali hiyo imefanya uongozi uanze kumsaka mrithi wake kwa kasi ya kimondo na tayari umefanya mazungumzo na viungo wengi ili mmoja wao azibe nafasi ya Mganda huyo aliyekuwa ‘dereva’ wa mashambulizi ya Simba.
Simba imefanya mazungumzo na Etekiama Taddy wa AS Vita Club ya DR Congo ambaye amekuwa mmoja wa wafungaji bora wa michuano ya Kombe la Kagame kwa kufunga mabao sita sawa na mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi.
Mwingine ni Allan Wanga, Mkenya anayekipiga katika klabu ya AFC Leopard ya Nairobi, Kenya, baada ya kurudishwa kwa mkopo na klabu ya Hoang Anh Gia Lai ya Vietnam. Wa tatu ni kiungo mwenye kasi wa timu ya taifa ya Uganda, Sula Matovu ambaye sasa ni tegemeo la ushambuliaji katika timu ya St George ya Ethiopia.
“Simba imefanya mazungumzo na viungo hao, wote wameonyesha nia ya kuja kuichezea. Ila kumekuwa na mambo kadhaa,” chanzo kilieleza.
“Simba wamepewa taarifa kwamba, Okwi anafanya vizuri sana, wakala wake ameiambia Simba ana takribani asilimia 90 za kufuzu.”
Championi Jumatano liliusaka uongozi wa Simba ambao ulikubali kwamba umefanya mazungumzo na viungo hao kwa nyakati tofauti.
“Kama Okwi ataondoka hatutakuwa na ujanja, lazima tuwe na mtu mwenye kasi. Video za wachezaji wawili, Wanga na Matovu, kocha ameziangalia na kukubaliana nazo, lakini yule wa AS Vita (Taddy) alimuona uwanjani,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
“Matovu tutazungumza naye tena hivi karibuni, AS Vita pia wapo tayari kwa ajili ya mazungumzo. Pia tunapanga kuzungumza na ile klabu ya Vietnam (Hoang Anh) kuhusiana na Wanga. Tumeambiwa Okwi anafanya vizuri na matumaini ya kufuzu yapo, ila kikubwa tunaendelea kusubiri jibu la uhakika kutoka katika klabu yenyewe.
“Tumeambiwa litapatikana baada ya wiki moja au mbili. Rasmi ameanza tena majaribio jana (juzi) Jumatatu. Alisimama kwa wiki moja baada ya kuugua malaria na hicho ndicho kimechelewesha majibu ambayo huenda tungeyapata wiki iliyopita,” alisema Kaburu.
Simba ilishindwa kucheza katika kasi yake wakati wa michuano ya Kagame kutokana na kutokuwa na mwanzisha mashambulizi kama alivyokuwa akifanya Emmanuel Okwi.
No comments:
Post a Comment