Na Lucy Mgina
MAJINA ya wachezaji watano wa Yanga likiwemo la mshambuliaji Jerry Tegete (pichani), yamewasilishwa kwenye dawati la Toto African tayari kwa kujiunga na timu hiyo kwa mkopo.
Ukiacha Tegete, wachezaji wengine ambao wamepelekwa kwa mkopo katika klabu hiyo ni Shamte Ally, Ibrahim Job, Godfrey Taita na Ladislaus Mbogo.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya klabu ya Toto kimeliambia gazeti hili kuwa, majina hayo bado yanafikiriwa kwa kuwa benchi la ufundi haliwataki baadhi ya wachezaji kutokana na uwezo wao kuwa mdogo.
Kiliongeza kuwa, mpaka sasa bado hawajafikia uamuzi wowote wa kuwachukua wachezaji hao, japokuwa wanajua ni vigumu wao kuwakataa wote kutokana na Yanga kuwalazimisha sana wawachukue.
“Kuna majina matano ya wachezaji wa Yanga walioletwa ili wacheze kwa mkopo msimu ujao, akiwemo Tegete lakini bado hawajafikia muafaka, nafikiri kwa kuwa dirisha la usajili limesogezwa mbele ndiyo maana wanafanya taratibu.
“Lakini kama unavyojua hawawezi kuchomoa, Yanga wanawang’ang’aniza sana na hawa ni kama ndugu fulani!” kilisema chanzo hicho.
Championi Jumatatu lilimtafuta Kocha wa Toto, Athuman Bilal, kumhoji kuhusiana na hilo na alipoulizwa alisema bado hajapewa taarifa yoyote na hajui kitu kuhusiana na wachezaji hao kama watapelekwa katika kikosi chake.
“Sijui lolote kuhusu hilo kwa kuwa sina taarifa kuhusiana na wachezaji hao kuletwa Toto,” alisema Bilal.
No comments:
Post a Comment