NAMSHUKURU Mungu kwa kunipa afya njema iliyoniwezesha kuyaandika haya niliyokusudia. Nimshukuru pia kwa kutufanya Watanzania watu wapenda amani; jamani tudumishe amani hii ambayo ni kitu cha thamani kama lulu kwa kila Mtanzania.
Leo nitajikita zaidi kujadili kile ambacho Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Anne Makinda amekitamka kwa kutoa ushauri wa bure kwa wabunge wa viti maalumu ambapo amesema kwamba, badala ya kuendelea kubweteka katika nafasi hizo, wajinasue sasa na kwenda kugombea majimboni kwani nafasi hizo zinawapotezea heshima mbele ya jamii.
Spika Makinda alitoa ushauri huo wiki iliyopita mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na wabunge wanawake kwenye mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha-Rose Migiro aliyekwenda kuwashukuru wabunge hao kwa mchango wao aliosema ulichangia kumwezesha kuwa na utumishi wenye ufanisi katika umoja huo.
Binafsi nimpongeze Spika Makinda kwa kuwazindua wabunge hao ambao hakika wanaonekana kulala usingizi wa pono na kuridhika na nafasi hizo za viti maalumu bungeni, huku wakisahau kwamba ni nafasi ambazo zinapaswa kurekebishwa ndani ya katiba kwa kuwa hazisaidii na hatutaki kuona wanawake wakipendelewa kwani wana uwezo mkubwa katika kazi za kijamii.
Mfano mzuri ni Makinda mwenyewe, amekuwa mbunge wa jimbo tangu mwaka 1975. Anastahili pongezi na ana wajibu wa kuwakumbusha wanawake wenzake kwamba enzi za kupendelewa zimepitwa na wakati sasa.
Ndugu zangu wabunge wa viti maalum, ushauri alioutoa mama Makinda ni wa nia njema na niseme wazi bila kumung’unya maneno kwamba umetolewa wakati mwafaka wakiwa wanakaribia katikati ya kipindi cha utumishi wao wa miaka mitano bungeni.
Spika katika ushauri wake wa bure anasema wabunge wa viti maalumu wanaonekana kuringa na kujisahau kabisa kwenda majimboni, huku akionya kwamba kitendo cha kuendelea kubweteka kitakuwa kimewaangusha wanawake wa Tanzania, ambao alisema wanategemea ushiriki wao katika chombo hicho muhimu cha kufanya maamuzi.
Hakika kwa mtu anayeona mbali na kufikiri, hayo ni maneno makali ambayo pengine yatakuwa yameudhi baadhi ya wabunge hao kwa madai ya kudhalilishwa lakini ukweli ni kwamba nafasi za viti maalumu watu wengi wanazipinga na naamini katiba ya nchi ijayo itapiga teke nafasi hizo za upendeleo katika ulimwengu wa leo ambao Tanzania tumetoa mwanamke kushika nafasi ya juu katika Umoja wa Mataifa.
Kusema kweli naiunga mkono kauli hiyo ya Spika Makinda kwa sababu imetolewa kwa nia njema ya kurekebisha mwenendo wa wabunge hao ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi wengi nchini, kwa kuwa hawana majimbo.
Nasema mama Makinda amepatia kutoa ushauri huo kwa kuwa tayari wananchi wengi wakati wa mijadala inayoendelea nchini kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania, wamesema hawaoni sababu ya viti hivyo kuwekwa kwenye katiba ijayo.
Inavyoelekea hapa ni kwamba Spika Makinda anajikuta katika hali ngumu kama mwanamke ambaye anataka wabunge wanawake wenzake bungeni watimize wajibu wao kwa ufanisi na kufuta dhana hasi inayoshikiliwa na baadhi ya watu kwamba wabunge wanawake siyo tu wanapendelewa, bali pia hawana uwezo naamini ndiyo maana anapenda wabunge waliokalia viti hivyo kwa muda sasa wajitayarishe kupambana majimboni ili wapate viti vya majimbo.
Japokuwa Spika Makinda anasema atapendekeza katiba mpya iruhusu asilimia 30 ya viti vya ubunge watengewe wanawake kama ilivyo sasa, lakini asilimia 20 nyingine watengewe wanawake watakaogombea majimboni, mimi naamini Watanzania wengi watataka kusiwepo hata asilimia moja ya viti maalumu, vya nini? Labda viwepo kwa walemavu.
Napenda kuwahamasisha wanawake kwenda kuomba kura kwa wananchi kama walivyofanya baadhi yao mwaka 2010. Hatua ya wapigakura kuwachagua wanawake katika chaguzi mbalimbali kama za udiwani au ubunge ni uthibitisho tosha kwamba wanawake wanaweza kushindana na wanaume bila kubaguliwa au kupendelewa.
Napendekeza kuwa huo ndiyo uwe msimamo wa wanawake wote nchini, na naamini baadhi wanakubaliana na hilo hasa wasomi, wanachama wa taasisi na vyama vya kijamii vinavyoshughulikia masuala ya wanawake, ikiwamo Tamwa. Kada hiyo pia inapinga uwepo wa viti maalumu na kusema wawakilishi wa wanawake bungeni kupitia viti hivyo mpaka sasa hawajasaidia kusukuma ajenda za wanawake.
Upo ukweli kwamba wapo wabunge wachache wa viti hivyo ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa bungeni, ingawa nao wameshindwa kuibua na kusimamia ajenda za wanawake na watoto.
Kutokana na hayo nihitimishe kwa kusema kuwa wabunge wa viti maalumu wanapaswa kuufanyia kazi ushauri wa Spika Makinda.
No comments:
Post a Comment