Na: Luqman Maloto
Mpenzi msomaji, wiki hii ni kwa walio ndani ya ndoa na wale wanaotarajia kuingia kwenye ndoa. Kudumu kwa ndoa siku zote kunahitaji nguvu ya ziada baina ya wawili waliopendana.
Ukiona ndoa ya watu flani imedumu kwa miaka mingi, si bure na ndiyo maana leo nimeona niwaletee mambo kadhaa ambayo yanaweza kuifanya ndoa yako idumu milele na milele.
Kwanza, jenga uaminifu kwa mwenza wako.
Uaminifu ni kitu cha msingi sana kwa wanandoa, unaposhindwa kumuamini mwenza wako, mara nyingi utakuwa ukihisi anakusaliti hata kama siyo kweli.
Hali hiyo inaweza kukufanya ukakosa amani kila mwenza wako anapokuwa mbali na wewe.
Si kukosa amani tu anapotoka au anapokuwa mbali na wewe bali pia anaporudi unaweza kushindwa kuonesha mahaba kwake na kujenga uhasama dhidi yake.
Suala la uaminifu limekuwa adimu sana kwa baadhi ya wanandoa.
Ni wachache sana ambao ni waaminifu kwa wanandoa wenzao. Wengine wakipewa umbeya kidogo tu kwamba mwenza wake anamsaliti anakubali mara moja na kuchukua hatua ambazo zinaweza kuteteresha ndoa yao.
Unachotakiwa kufanya ni kuamini kwamba mwenza wako ni mwaminifu kwako na jijengee mazingira ambayo na yeye ataamini wewe ni mwaminifu kwake.
Muamini ili naye akuamini. Epuka sana kufanya mambo ambayo yanaweza kumsababishia mwenza wako kudhani unamzunguka kwenye ndoa.
Waweza kufanya hivyo kwa kuwa makini na maneno yako pamoja na matendo yako ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kudhihirisha kwamba si mwaminifu katika ndoa.
Kitendo cha kuchelewa kurudi kazini kila siku bila kuwa na sababu za msingi, kulala nje, kuwa na uhusiano wa karibu na watu wa jinsi tofauti bila kuwepo na sababu za msingi, kupunguza mapenzi, kutokuwa na heshima ni baadhi ya matendo ambayo yanaweza kuonesha kwamba si mwaminifu hivyo ni vyema ukaepukana navyo.
Pili, epuka mabishano yasiyo ya lazima ndani ya ndoa. Kimsingi watu wanatofautiana kitabia. Kuna wengine wana tabia ya ubishi hata kama jambo linalozungumziwa halistahili kubisha.
Kama utakuwa na tabia hiyo basi ni vyema ikaishia nje ukiwa na marafiki zako lakini si kwa mwenza wako.
Unapokuwa na tabia ya kubishana na mpenzi wako hata katika kile ambacho hakistahili kubisha, unakaribisha mazingira ya kugombana.
Kama kweli unataka kuona ndoa yenu inakwenda vizuri, jifunze ukweli kwamba si kila wakati unaweza kuwa sahihi, kuna wakati utakuwa haupo sahihi na inapotokea hivyo, kubaliana na hali halisi.
Inapotokea kwamba kweli umefanya kosa halafu unabisha kwamba haukufanya, ni hatari sana.
Kama umekosea kubali kosa kisha omba radhi.
No comments:
Post a Comment