Na Khatimu Naheka
SIKU chache baada ya kuanza kazi ya kuinoa timu yake mpya ya Azam FC, kocha wa timu hiyo, Boris Bunjak ‘Boca’ amesema kuondoka kwa winga machachari Mrisho Ngassa hakujaacha pengo katika kikosi hicho.
Ngassa aliondoka Azam na kusaini mkataba Simba Agosti 2, mwaka huu kwa dau la jumla ya shilingi milioni 73 ukijumlisha gari, Sh milioni 30 alizopewa na 25m zilizokwenda kwa watengeneza ice cream hao.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Bunjak alisema winga huyo hana madhara makubwa kutokana na kutumia mbio pekee kama silaha yake kubwa, mbinu ambayo ni rahisi kukabwa na beki yeyote mzuri.
Bunjak alisema hakuna pengo kufuatia kuondoka kwa winga huyo na kusisitiza kuwa angepata tabu kama kiungo Abubakar Salum ‘Sure Boy’ angetimka katika timu hiyo lakini siyo Ngassa.
“Ngassa ni mchezaji mzuri lakini binafsi sidhani kama klabu itapungukiwa chochote, nimemuona akicheza akiwa na Simba lakini amebarikiwa mbio pekee, mbinu ambayo akikutana na beki ambaye hatampa nafasi ya kukimbia na mpira, hawezi kucheza,” alisema Bunjak.
“Nimeiona Azam FC, bado ina wachezaji hatari zaidi ya Ngassa, kama yule anayevaa jezi namba nane ‘Sure Boy’ na (John) Bocco wangeondoka, ndiyo timu ingeyumba kutokana na vipaji vyao kuwa vya kipekee,” aliongeza raia huyo wa Serbia.
No comments:
Post a Comment