Tuesday, July 24, 2012

yanga yafanya mambo

Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet.
Na Khatimu Naheka
UONGOZI wa Yanga umempa kocha wao Tom Saintfiet, kazi ya kutafuta wachezaji wawili watakaojaza nafasi ya Davies Mwape na Kenneth Asamoah.
Taarifa zinaeleza, Yanga itapata washambuliaji hao wawili kutoka Nigeria na Kenya kwa ajili ya kuongeza nguvu ya mashambulizi.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, amekiri kuwa benchi la ufundi limeonyesha linahitaji washambuliaji wawili ‘hatari’ na tayari kocha Saintfiet amekabidhiwa jukumu hilo.
“Kweli Yanga inataka washambuliaji wawili na kazi tumempa kocha, yeye anaweza kujua,” alisema Manji.
Hadi sasa Yanga imebakiza nafasi mbili za kujaza kabla ya kukamilisha usajili Agosti 10.
Akizungumza jana na Championi Jumatatu, Saintfiet raia wa Ubelgiji, alisema tayari alishaanza mchakato huo wa kutafuta wachezaji hao ambapo anataka kuhakikisha timu hiyo inapata wachezaji walio katika viwango bora hasa katika safu ya ushambuliaji ili wasaidiane na Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Saintfiet alisema tayari ameshapata majina machache ambayo hawezi kuyaweka wazi sasa lakini kalidokeza kidogo Championi Jumatatu kuwa kuna uwezekano mkubwa akaleta nyota kutoka Nigeria ambako alikuwa akiishi kabla ya kuja Yanga pamoja na Kenya ambako kumeonekana kuna washambuliaji wazuri.
“Ni kweli nimepewa majukumu hayo ya kutafuta wachezaji wawili ambao wataziba nafasi mbili na tayari nilishaanza kazi hiyo mapema na nilikuwa naangalia pia katika michuano hii ya Kombe la Kagame na nimeona baadhi lakini bado naendelea na mchakato huo tararibu,” alisema Saintfiet.
“Najua bado muda ninao lakini unajua mimi nina uzoefu mkubwa katika nchi za Bara la Afrika. Nina marafiki wengi, nataka nikwambie nimeshafanya mipango katika nchi za Nigeria na Kenya ili kupata wachezaji bora wasaidiane na hawa kina Bahanuzi na Tegete ili kuhakikisha safu ya ushambuliaji inakuwa na makali zaidi,” aliongeza.
Taarifa nyingine za ndani za Yanga zinaeleza huenda Saintfiet akatupa jicho nchini Zimbabwe pamoja na kuangalia baadhi ya washambuliaji wanaoshiriki michuano ya Kagame, huku mmoja akielezwa anatoka Burundi.
Uamuzi wa Yanga kutafuta mshambuliaji umepitishwa baada ya timu hiyo kucheza mechi za kirafiki pamoja na zile za mwanzo za michuano ya Kagame.
Safu ya ushambuliaji imeonyesha kupwaya na sasa inamtegemea Bahanuzi ambaye alijiunga Yanga akitokea Mtibwa Sugar alikokuwa akicheza kama winga.
Mshambuliaji Jerry Tegete ameshindwa kuonyesha cheche tangu kuanza kwa michuano hiyo na imekuwa moja ya sababu zilizowashtua Yanga waanze kuhaha tena kusaka washambuliaji wenye njaa na mabao.

No comments:

Post a Comment