Marehemu Agnes B. King’unza enzi za uhai wake.
Mwili wa Marehemu Agnes ukiwa kanisani kwa heshima za mwisho.
Mama mzazi wa Agnes akilia kwa uchungu baada ya kuona mwili wa mwanae.
Baba mzazi wa marehemu Agnes, Bwana Bernard King’unza (mwenye koti jeusi kulia).
Baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma na marehemu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Haruni Sanchanwa na Makongoro Oging’MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu Cha Usimamizi wa Fedha, (IFM) jijini Dar es Salaam, Agnes B. King’unza (pichani), amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuokotwa akiwa hajitambui katika ufukwe wa Bahari ya Hindi jirani na Coco Beach.
Habari za kipolisi zinasema Agnes alitekwa kisha akaokotwa na msamaria mmoja ambaye kwa taarifa za awali anatajwa kuwa ni mlinzi wa nyumba moja maeneo ya Coco Beach, ambako ndiko alikokutwa akiwa hajitambui.
“Polisi na hata watu wengine wanahisi kuwa msichana huyo alitekwa kisha kutupwa na watu wasiofahamika, baada ya kufanyiwa ukatili wa kutisha kwa kunyweshwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu,” kilisema chanzo chetu cha habari ndani ya jeshi la polisi.
Habari zinasema baadaye mwanafunzi huyo ambaye alikuwa akichukua shahada ya mambo ya kodi, alipelekwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay kisha askari hao wakamkimbiza Hospitali ya Agha Khan kwa matibabu.
Hata hivyo, habari zinasema madaktari wa Agha Khan baada ya kuona hali ya mgonjwa ilikuwa mbaya, walimpa rufaa na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
“Agnes alifariki jioni ya Julai 16, mwaka huu katika Hospitali ya Muhimbili na habari za kifo chake zilisababisha Chuo cha IFM kuzizima kwa wanafunzi kumlilia mwenzao,” kilisema chanzo hicho.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema kwamba wasamaria wema walisema waliona Bajaj ikifika eneo alilotupwa Agnes wakadhani wanatupa mzigo.
“Walipokwenda kuangalia wakakuta ni mtu akiwa hoi hajitambui. Baada ya kupelekwa hospitali siku ya pili alikuja mama mdogo wa marehemu Agnes aitwaye Veronica Galus na akaleta taarifa kuwa binti yao huyo amefariki dunia. Polisi tunaendelea na uchunguzi kuwatafuta wahusika,” alisema Kenyela. Hata hivyo, kifo hicho kimeacha maswali mengi kuwa binti huyo alilishwa nini na nani?
Mzazi wa marehemu aliyetajwa kwa jina la Bernad King’unza mkazi wa Kimara Dar, hakupatikana kwa maelezo kwamba alikuwa safarini Iringa kwenye mazishi ya mpendwa wao huyo yaliyofanyika nyumbani kwao Kalenga, Iringa Julai 19, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment