Na Haruni Sanchawa
SIKU chache baada ya serikali kutangaza kusitishwa kwa zoezi la uopoaji wa miili katika meli ya Skagit iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe, baadhi ya wananchi wamerusha lawama kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kwamba ina upungufu katika utendaji wao wa kazi.
Wakizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita baadhi ya wananchi walisema kumekuwa na mchanganyiko wa idadi ya abiria kila meli inapopata ajali, hali inayoonesha kwamba Sumatra hawana utaratibu mzuri wa kuelekeza wamiliki wa vyombo vya majini jinsi ya kutunza kumbukumbu za abiria wanaopanda melini.
“Hakuna utaratibu mzuri wa kutunza kumbukumbu wanaoingia katika meli na hii inachangia watu wengi kuingia katika chombo bila shaka kupita uwezo wake.” Alisema Saidi Kilopwa Saidi aliyekuwa akisafiri kwenda Zanzibar aliyekuwa bandarini Dar es Salaam.
Naye Maulidi K. Mohammed alisema vyombo vingi vya usafiri wa majini hapa nchini hasa meli za abiria ni kuukuu. “ Serikali zetu zote mbili hazina mpango wa kununua meli mpya na Sumatra wapo na hawatoi ushauri wowote, wanategemea nini?” alihoji Mohammed.
Kwa upande wake Sofia Mohamed Tamim alisema ushahidi kwamba meli za abiria nchini zimezeeka upo wazi. “Analia meli ya MV Liemba. Ni ya mwaka 1913 kabla ya watu wote hapa unaowaona hawajazaliwa lakini meli inabeba abiria kule Kigoma, serikali inangoja watu wafe?” alihoji Sofia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sumatra, meli hiyo iliyozama ni mali ya Kampuni ya Seagul Transport, imesajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na kwamba, Cheti cha Ubora kimeanza Agosti 23, 2011 na kinamalizika Agosti 24, 2012.
Taarifa ya Sumatra ambayo gazeti hili inayo inasema meli hiyo ilikuwa imeruhusiwa kubeba abiria 300 na tani 26 za mizigo, hata hivyo kwa mujibu wa habari za awali za kipolisi, meli hiyo ilikuwa na watu zaidi ya 400.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alisema serikali inajipanga ili kuhakikisha kuwa ajali kama hiyo haitokei tena. “Tunajipanga kuhakikisha hali kama hii haitokei tena kwa sababu inatia huzuni sana kuona watu wakifa kila mara kwa ajali za meli,” alisema Nchimbi.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18, 2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar.
No comments:
Post a Comment