MUNGU ni mwema sana, bado anatupenda ndiyo maana tumekutanika tena leo katika safu hii. Hakika anapaswa kuabudiwa na kila binadamu.
Baada ya kusema hayo leo nizungumzie kwa masikitiko makubwa na huzuni juu ya ajali za meli zinazotokea nchini ambazo sasa ni kama utamaduni unaojirudia kwani zinaua watu wengi wasio na hatia.
Baada ya miili ya abiria wapatao 50 kuopolewa wakiwa wamefariki dunia na wengine 137 kuokolewa wakiwa majeruhi kutokana na meli ya Skagit iliyokuwa imebeba abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kuzama wiki iliyopita karibu na Kisiwa cha Chumbe, kilomita 19 kutoka Bandari ya Malindi, mjini Zanzibar, nchi nzima imejaa majonzi.
Nchi yetu sasa imekuwa ni ya misiba mbaya zaidi ni kwamba haipiti miezi mingi kabla vyombo vya habari havijatangaza habari za vifo vya mamia ya watu vinavyotokana na ajali .
Ajali za vyombo vya majini, kama ilivyo kwa vyombo vya safari za barabarani, anga na reli zimezidi kuongezeka na kujenga dhana miongoni mwa wananchi kuwa, siyo tu ajali zimekuwa sehemu ya utamaduni wetu, bali pia kwamba ajali hizo kamwe haziepukiki.
Hii ni ajali ya pili mbaya kutokea visiwani humo katika kipindi cha miezi 10 tu tangu ilipotokea ajali nyingine ya MV Spice Islander Septemba 2011 ambapo watu wapatao 240 walikufa na wengine zaidi ya 1,500 hawajulikani walipo hadi leo baada ya meli hiyo kuzama katika Mkondo wa Nungwi ikiwa safarini kuelekea Pemba ikitokea Bandari ya Malindi, Unguja.
Rais Mohammed Shein wa Zanzibar aliunda tume kuchunguza ajali hiyo ikatoa ripoti iliyosema kuwa, meli hiyo ilikuwa imebeba mizigo na abiria kuliko uwezo wake.
Sote tujiulize, tumeshindwa kupata dawa ya kupunguza, kama siyo kukomesha ajali hizo zinazopoteza maisha ya Watanzania wenzetu wasio na hatia? Kwa nini meli ibebe abiria au mizigo kuliko uwezo wake? Hakuna vyombo vya serikali vya kuhakiki hilo?
Zipo taarifa kutoka shirika moja la kimataifa kuwa, meli hiyo iliyozama wiki iliyopita ilinunuliwa mwaka 2011 kutoka Marekani, lakini wataalamu walionya mwaka 2006 kwamba ilikuwa haifai tena kubeba abiria.
Ndugu zangu, kuna uzembe katika kuhakikisha usalama wa meli za abiria au hata za mizigo hapa nchini. Ipo mifano ya wazi, kwa mfano historia inaonesha kuwa
MV Bukoba ilizama katika Ziwa Victoria mwaka 1996 na kuua watu 1,000 kutokana na kujaza abiria na mizigo kupita kiasi.
Katika ziwa hilohilo kuna meli ya MV Victoria iliyoanza kutumika tangu miaka ya 60, imechakaa lakini bado serikali haichukui hatua, je mnasubiri izame na kuua maelfu ya abiria? Bila kuchukua hatua sasa meli hii wakati wowote inaweza kuzama kutokana na kuzeeka kupita kiasi.
Nayo Meli ya MV Liemba ambayo wakati wa wakoloni wa Kijerumani ilikuwa ikiitwa Graf Von Gotzen ilitengenezwa mwaka 1913 kabla ya kubadilishwa na kuwa na jina hilo mwaka 1927, ni kuukuu sasa, haifai kubeba abiria hata kama inakarabatiwa, lakini bado inabeba abiria na ni tegemeo Ziwa Tanganyika.
Tukumbushane tu kwamba hukohuko Zanzibar Mei mwaka huu, abiria wapatao 300 walinusurika kufa baada ya meli kushika moto katika eneo la Nungwi ulioanzia kwenye injini wakati ikielekea Unguja kutoka Pemba.
Hizi meli hazifai zitatuletea maafa siku si nyingi zijazo. Wakati umefika kwa vyombo vya serikali vinavyohusika na usalama wa abiria na mali zao kwenye meli kufanya uamuzi mgumu wa kuchukua hatua stahiki dhidi ya vyanzo vya ajali hizo na kusimamia sheria za usafirishaji.
Wala siyo sifa kwa viongozi wetu kuwa vinara wa kutoa rambirambi kwa wafiwa pindi ajali zitokeapo, badala yake wahakikishe ajali hizi zinaepukika.
Niseme wazi tu kwamba vifo vingi vinavyotokana na ajali hizo vimetokea kwa sababu vyombo vya serikali vinavyosimamia usafiri wa majini vimeshindwa kutimiza wajibu wake.
Kudhihirisha hilo ni kwamba kila ajali ya meli inapotokea kunakuwa na mkanganyiko kuhusu idadi kamili ya watu waliokuwa katika meli, hata ajali ya wiki iliyopita tulishuhudia mamlaka husika zilikitoa kauli zilizokuwa zinatofautiana au kukinzana. Hili ni tatizo.
Jambo moja linalojitokeza hapa ni kwamba baadhi ya meli zinazosafirisha abiria katika maziwa na bahari zetu siyo salama na hazifai tena kwa sababu zimechakaa, hivyo kugeuka vyuma chakavu.
Inashangaza kuona serikali zetu mbili za Muungano na Zanzibar hazioni umuhimu wa kununua meli mpya zilizo salama kwa ajili ya usafiri wa wananchi.
Tunazishauri serikali zote mbili zitambue kwamba majuto ni mjukuu, kwa maana ya kuhakikisha vyombo vya usafiri vinakuwa salama badala ya kusubiri kutokea kwa ajali na kuwa wepesi wa kutoa rambirambi. Hata wahenga walisema, kinga ni bora kuliko tiba. Kwa nini hatujifunzi kutokana na makosa?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment