Na Khatimu Naheka
MNYAMA Simba jana ameshikwa sharubu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kushindiliwa mabao 3-1 na Azam katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Kagame.
Shujaa wa Azam alikuwa ni John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao matatu ‘hat trick’ katika dakika ya 17, 46 na 74, lakini Simba walipata bao pekee la kufutia machozi katika dakika ya 53 kupitia kwa Shomari Kapombe.
Dakika ya nane ya mchezo huo ambao Simba walielemewa kwa kiasi kikubwa, Kipre Balou aliumizwa vibaya na Felix Sunzu ikabidi atoke dakika nne baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Dakika moja baada ya mabadiliko hayo, Simba walipoteza nafasi ya wazi baada ya shuti ya Uhuru Selemani aliyeunganisha pasi ya Sunzu kwenda nje kidogo ya lango.
Simba walifanya shambulizi la nguvu katika dakika ya 23, baada ya Uhuru Selemani kufanya kazi nzuri ya kuwatoka mabeki wa Azam na kumpa pasi Sunzu aliyemtengea Shomari Kapombe ambaye alishindwa kufunga baada ya shuti lake kwenda juu ya lango.
Dakika ya 35 Azam walikaribia kupata bao baada ya Tchetche kupiga kichwa safi akiunganisha krosi ya Erasto Nyoni lakini kipa Juma Kaseja aliutoa mpira na kuwa kona ambayo haikuwa na manufaa yoyote.
Msako wa mabao wa Azam uliendelea katika dakika ya 43, baada ya Bocco kuuvunja mtego wakuotea wa mabeki wa Simba na kubaki yeye na Kaseja, lakini kipa huyo alifanya kazi ya ziada kuuwahi mpira na kuutoa nje.
Sunzu nusura aipatie timu yake bao katika dakika ya 56, lakini mpira wa kichwa aliopiga akipokea pasi ya Kazimoto haukuwa na madhara kwenye lango la Simba.
Hata hivyo, huu ni mchezo wa tatu kwa Simba kukutana na Azam ndani ya mwezi mmoja baada ya kukutana kwenye michuano ya Ujirani Mwema mara mbili, ya kwanza walitoka sare na katika fainali Simba ikashinda kwa penalti.
Vikosi vilikuwa hivi: Simba; Kaseja, Shamte, Kapombe, Musombo, Nyosso, Mudde/Kinje, Uhuru/Kigi, Kazimoto, Boban, Sunzu na Gerrard/Kiemba.
Azam: Deogratius Munishi ‘Dida’, Ibrahimi Shikanda, Nyoni, Morad, Morris, Balou/Redondo, Tchetche, Sure Boy, Bocco, Mwaipopo na Mcha/Jabir.
Katika mchezo wa kwanza, Vita Club ya DR Congo ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga Atletico ya Burundi mabao 2-1. Mabao ya washindi yalifungwa na Etikiana Teddy dakika ya saba na Basijua Makola (92), wakati Atletico walipata bao lao kupitia kwa Pierre Kwizera (49).
Kutokana na matokeo hayo, Azam itavaana na Vita Club kesho mchana kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam wakati baadaye saa 10:00 jioni Yanga itakipiga na APR kwenye uwanja huo.
No comments:
Post a Comment