Na Saleh Ally
WAKATI Yanga ikiwa na matumaini ya kumnasa mshambuliaji hatari wa Polisi Rwanda, Mohammed ‘Meddie’ Kagere ambaye mkataba wake unamalizika mwezi huu, taarifa zinaeleza ametimkia nchini Afrika Kusini, huku kocha wa Wanajangwani hao akiwa mbogo.
Taarifa za uhakika ambazo zimethibitishwa na Mwenyekiti wa Polisi Rwanda, Alphonce Katerebe, zimeeleza Kagere ameondoka nchini humo wiki iliyopita kwenda Afrika Kusini.
“Kweli ametuambia amepata timu ya kufanya majaribio. Sijajua anakwenda timu gani ila nilisaini barua ya kuonyesha anaruhusiwa kwenda kufanya majaribio maana tunakaribia kumaliza naye mkataba,” alisema ofisa huyo.
Taarifa zinaeleza Kagere ameondoka jijini Kigali kwenda Afrika Kusini akiongozana na kiungo nyota wa APR, Papii Fatii, raia wa Burundi ambaye hakuja katika michuano ya Kagame.
Kagere alianza mazungumzo na Yanga mwezi uliopita, wiki chache zilizopita alitua jijini Dar es Salaam kumalizana na viongozi wa Yanga.
Hata hivyo, inaonekana hawakufikia mwafaka na Yanga ilisisitiza itaendelea kufanya naye mazungumzo.
Iwapo atapata timu Afrika Kusini, itakuwa ni pigo kwa Jangwani ambao wameona wana pengo kubwa katika safu ya ushambuliaji hali iliyomlazimu kocha, Tom Saintfiet (pichani), kumtumia kiungo Said Bahanuzi (pichani mbele) kufanya kazi hiyo.
Wakati huohuo, John Joseph anaripoti kuwa kocha wa Yanga, Tom Saintfiet amekuwa mkali na kuwalaumu wasiokuwa na faida kwenye timu hiyo huku akisema atawauza au waondoke wenyewe
Saintfiet alisema hayo mara baada ya mechi dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga kushinda kwa penalti 5-3 baada ya sare ya mabao 1-1 katika muda wa dakika 90.
“Siwezi kuwavumilia wachezaji ambao hawana faida katika timu, nitawauza. Sitaki wachezaji wanaokaa benchi bila kuwa na matunda kwenye timu yangu. Hata kama ukiwa benchi ukiingia unatakiwa uonyeshe kiwango,” alisema Saintfiet, kauli ambayo inaweza kuwagusa Jerry Tegete na Idrissa Rashid ambao waliingia lakini hawakuonyesha cheche.
“Yanga siyo klabu ya kuvaa jezi ya njano na kijani kisha unakaa benchi tu, nitawapatia barua zao za kuwaondoa hivi karibuni, sitaki wachezaji wa aina hiyo,” alisema Saintfiet huku akionekana kuwa na hasira.
No comments:
Post a Comment