Ndugu zangu,
Waziri
Muhongo ameusema ukweli wake kule Dodoma. Nami nimefuatilia sinema hii
ya Dodoma, kila inavyoendelea ndivyo ninavyozidi kuchoka. Ama hakika,
tunakokwenda siko, tuna lazima ya kujipanga upya.
Namsifu
Waziri Muhongo kwa ujasiri wake. Amutusaidia sana kuyajua yale ambayo
yangetuchukua muda mrefu kuyajua. Kwa kusimama kwenye ukweli Waziri
Muhungo ameitendea haki nchi yetu tuliyozaliwa.
Na
tulipofikia hapa ni ukweli tu ndio utakaotusaidia kutupa ahueni ya hali
mbaya tuliyonayo kama taifa. Huu si wakati wa kutanguliza siasa za
vyama bali kuitanguliza Nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda.
Kutanguliza uzalendo.
Leo
tunabaki vinywa wazi kusikia kuwa hata wachungaji, na wengine
wamejiingiza Bungeni, kuwa nao wanawaibia Watanzania wenzao. Kwamba nao
hawatosheki. Wanaiba huku wakitaja neno la Mungu. Leo hata wale
wanaojinadi kuwa ni watetezi wa wanyonge wameanza kutiliwa mashaka.
Uwezo wao wa kiuchumi unahusianishwa na ' madudu' kama haya ya Tanesco.
Na kuna hata wenye ' kuwafuturisha' wenzao wenye uwezo kwa fedha
walizowaibia wananchi wanyonge. Hawa hawana cha swaumu bali wanashinda
na njaa kwa dhambi ya wizi wao.
Tuna
lazima sasa ya kuamka na kuwabana wezi wetu. Mwizi ni mwizi tu, hata
kama ni mheshimiwa Mbunge.Na ukweli ndio unaohitajika sasa. Na si nusu
ukweli, bali ukweli mzima hata kama utatugharimu maisha yetu.
Nimepata kusimulia kisa cha kijana aliyehangaika sana kuusaka ukweli. Katika pitapita zake akaliona duka. Kibao kimeandikwa dukani ; ” Hapa tunauza ukweli”.
Dukani hapo ukweli unauzwa kwa kilo. Bei ya robo kilo ya ukweli imeandikwa, vivyo hivyo, bei ya nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya ukweli mzima, kwa maana ya kilo nzima ya ukweli.
Kijana yule akauliza; ” Mie nataka ukweli kilo nzima, mbona hujaandika bei?”
” Alaa, unataka kilo nzima ya ukweli?” Aliuliza mwenye duka.
” Naam” Akajibu kijana yule.
” Basi, zunguka uje ndani nikuambie bei yake”.
Alipoingia ndani dukani, kijana yule akaambiwa;
” Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima ni uhai wako. Je, uko tayari?”
Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima.
Katika Uislamu inasemwa; sema ukweli, hata kama unauma na kwamba unaweza kupelekea umauti wako.
Hakika, maandiko ya kwenye vitabu vya dini zetu hizi yana ya kutufundisha.
Na hilo ni Neno langu la Leo.