Saturday, June 16, 2012

MRADI WA VIJANA

Kibaha watangaza mradi wa viwanja  
Mwandishi Wetu
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha imeanzisha mpango kabambe wa makazi bora na kwa kushirikiana na  Kampuni ya Kibaha Golf Course Estate Development, imepima viwanja 169  vya makazi na biashara.

  Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Jenifer Christian, alisema viwanja hivyo vitaanza kuuzwa wiki ijayo.

Alisema viwanja hivyo viko katika eneo la Pangani, kilometa 4.5 kutoka Barabara ya Morogoro na kilometa 1.5 kutoka eneo jipya la biashara la mji wa Kibaha.

Taarifa hiyo ilisema huduma za umeme zipo umbali wa kilometa 1.5 kutoka katika  viwanja hivyo na kwamba kuna mkakati wa  kufikisha nishati hiyo kwenye eneo la  mradi.
"Wananchi, kampuni na taasisi zinazohitaji viwanja wanakaribishwa kufika ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Kibaha kuanzia Mei 28, ili kuchagua kiwanja kwenye ramani zitakazokuwa zimebandikwa kwenye mbao za matangazo," ilisema taarifa  ya mkurugenzi huyo.
Taarifa hiyo ilisema mwombaji anapaswa kulipa Sh 10,000 kama ada ya maombi na asilimia 25 ya gharama za kiwanja atakachochagua.
“Viwanja vya makazi vinauzwa kwa Sh7,500 kwa mita moja ya mraba na viwanja vya biashara ni  Sh8,500 kwa mita moja ya mraba,” ilisema taarifa. 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mradi wa Kampuni ya Kibaha Golf Course Estate Development iliyopima viwanja hivyo, Gaston Sanga, alisema viwanja 159 ni vya makazi na 10 ni kwa ajili ya makazi na biashara.

No comments:

Post a Comment