Mnyika atimuliwa bungeni kwa kusema Kikwete dhaifu
John mnyika akitoka njee ya ukumbi |
John Mnyika akiwa njee ya Bunge |
Tuesday, 19 June 2012 21:40
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
akiingizwa na askari wa bunge kwenye gari baada ya Naibu Spika, Job
Ndugai kuamuru atolewe nje ya viwanja vya bunge baada yambunge huyo
kugoma kufuta kauli yake kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, wakati
akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13,
mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mussa Juma, Dodoma na Fedelis Butahe, Dar
BUNGE jana lilichafuka tena baada ya
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kusema kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu,
kauli ambayo ilisababisha Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru atolewe
bungeni.
Mnyika alitoa kauli hiyo wakati
akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13, ambapo
alieleza kuwa analazimika kusema Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, wabunge
ni wazembe na nchi imefika hapa ilipo kutokana na upuuzi wa Chama cha
Mapinduzi (CCM).
"Mimi nasikitishwa na jambo moja,
tumefika hapa kutokana udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa bunge na
wabunge na tumefika hapa kutokana na upuuzi wa CCM, nasema hivi nina
ushahidi.”
Lukuvi/ Ndugai
Kauli hiyo ya Mnyika ndio ilichafua hali
ya hewa bungeni, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na
Uratibu, William Lukuvi ndipo alisimama na kuomba mwongozo wa Spika.
“Nataka kumbukusha Mnyika, kutokana na
kauli zake, kwa kutumia kanuni ya 64 (d) ambayo inaeleza mbunge yeyote
hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kulishawishi bunge
kwa jambo lolote,” alisema Lukivi.
Aliendelea kufafanua kuwa, “Lugha kwamba
Rais Kikwete ni dhaifu, CCM ni wapuuzi nilikuwa naomba, Mheshimiwa
Mnyika, miongoni mwa watu ninaowaheshimu sana, nadhani katika hili,
amepotoka naomba afute kauli yake.”
Baada ya kauli hiyo ya Lukuvi, Ndugai
alifafanua zaidi kuhusu jambo hilo akisema ni kweli kanuni inajieleza
vizuri sio tu katika maneno yake pia amelisema vibaya Bunge hilo na
kumtaka afute kauli hiyo.
Mnyika alisimama na kuomba apewe nafasi
ya kufafanua kauli yake ya kwanini Kikwete ni Rais dhaifu, lakini Naibu
Spika, alimuomba afute kauli yake, kitu ambacho mbunge huyo aligoma
kufanya, badala yake akasisitiza bunge limpe nafasi ya kufafanua.
Kutokana na uamuzi wa kumtimua Mnyika bungeni.
Ndugai alisema mbunge anapotoa lugha ya
matusi au maudhi na akatakiwa na kiti cha Spika afute kauli yake na bado
akagoma, ni mamlaka kwa kiti hicho kumtoa nje ya bunge katika muda
uliosalia au hata kumsimamisha asihudhurie vikao vitano vya bunge.
Ndugai aliamuru walinzi wamtoe Mnyika nje mara moja na kumzuia asishiriki shughuli yoyote ya bunge hadi kesho saa 3:00 asubuhi.
“Ndugu wabunge tunaongozwa kwa
utaratibu, nikitoa uamuzi wangu kwa Kanuni ya 73 (2), ambayo inaeleza
kuwa, mbunge au waziri atakayetoa lugha ya maudhi atatatakiwa na Spika
ajirekebishe na akikataa atakaa nje kwa muda wote ulisalia katika kikao
cha siku hiyo. Nikiwa Naibu Spika ninayejiamini, uamuzi ambao nauchukua
sasa, Askari mliopo hapa naagiza mumtoe nje mheshemiwa Mnyika mara
moja,” aliagiza Ndugai.
Kabda ya tukio hilo, Mnyika alichangia
bajeti hiyo kwa maneno makali dhidi ya wabunge wa CCM wanavyopigania
bajeti ya Serikali isiyotekelezeka, huku akiwafananisha na mtu asiye na
akili timamu (chizi), kwamba yeye akiendelea kupambana nao ndio
ataonekana chizi zaidi.
“Mtu ukiwa unamkimbiza chizi wewe ndio
utaonekana chizi zaidi, hivyo siungi mkono na waache machizi waendelee
na uchizi wao,” alisema.
Kauli hiyo ya Mnyika inaonekana kutaka
kujibu mapigo ya kikao cha juzi ambapo mbunge wa Iramba Magharibi (CCM),
Mwigulu Nchemba wakati akichangia bajeti, alisema kuwa wapinzani ni
wanafiki, waongo, wana mapepo na wanapaswa kuombewa na kupimwa akili.
Alisema bajeti hiyo haiendani na Mpango
wa Taifa wa Miaka Mitano, ambao ulisainiwa na Rais Kikwete na pia
haiendani na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo akashangaa kauli za wabunge
wa chama tawala kuishambulia Bajeti ya Upinzani kwa maneno ambayo
aliyasema anaweza kuyafananisha na uchizi.
“Wanasema mipango, unafikia kusema
maneno mengine ni ya uchizi uchizi, hivi kutokana na maeneno
yaliyotekelezwa, kama ya upinzani haitekelezeki, lakini tumezungumza
pensheni ya wazee katika bajeti iliyopita, kwa bahati mbaya wabunge hawa
wa CCM sijui hamuwasikilizi hata viongozi wenu?" alihoji Mnyika.
Alifafanua kuwa ,"Suala la malipo ya
pensheni kwa wazee, hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kulizungumza
mjini Morogoro katika sherehe za wazee, na aliahidi Serikali itakwenda
kutoa pensheni ya wazee. Sasa hapa unaposema haitekelezeki ndio maana
unafikia kusema kuna kauli nyingine kama ni za uchizi uchizi hivi."
Alisema pia katika suala la ongezeko la
mishahara hadi kufikia 315,000, wamerudia katika bajeti ya upinzani
kwani linawezekana, sitaki kutaja hapa takwimu za wafanyakazi wote wa
Serikali na malipo yao.
“Lakini, bunge lililopita tulitoa
takwimu hapa jinsi ambavyo inawezekana mshahara kima cha chini ufikie
315,000 na ndio sababu leo tumerudia tena, kwani Serikali haijatekeleza,
lakini kuna wapofu wa kumbukumbu ambao hawasomi kumbukumbu za bunge,"
alisema Mnyika.
Nje ya Bunge
Baada ya agizo hilo la Ndugai, askari wa
bunge walimwondoa Mnyika na kumsindikiza hadi nje ya uzio wa bunge,
ambako alizungumza na wanahabari na kufafanua kuwa, alisema Rais Kikwete
ni dhaifu kutokana na sababu ambazo alikuwa nazo, ila hakupata nafasi
ya kuzitaja.
Alisema sababu hizo zilitokana na bajeti
ya Serikali ambayo ilisomwa bungeni, ambayo haitekelezeki na inakinzana
na Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka
mitano.
“Bajeti hii ni matokeo ya udhaifu wa
Rais Kikwete, narudia tena kwani yeye ndiye aliyesaini Mpango wa Taifa
wa Maendeleo wa miaka mitano kama Kiongozi Mkuu wa nchi tena kwa wino
mwekundu, mpango ambao sasa unapingana na bajeti hii,” alisema.
Alisema pia Rais Kikwete ni dhaifu kwani
ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na bajeti ilipita katika baraza
hilo, lakini imedhihirika kwamba haikuzingatia kuzingatia mpango wa
maendeleo, pia kushindwa kutekelezwa kwa bajeti iliyopita ni matokeo pia
ya udhaifu.
"Mnyika alisema pia kwa mujibu wa
Katiba, Rais ndiye anapeleka bajeti bungeni, Waziri mwenye dhamana
anapeleka tu kwa niaba. Hivyo Rais amepewa mamlaka makubwa juu ya
bajeti, hivyo Rais Kikwete anapaswa kuagiza Waziri wa Fedha bajeti
iondolewe irudi kwenye Baraza la Mawaziri ikafanyiwe marekebisho kama
atataka," alisema.
Hata hivyo, alisema kutokana na ubovu wa
Katiba, michango ambayo inaendelea sasa bungeni, haitaweza kupinga
bajeti kwani inatakiwa ipitishwe kwa kupiga kura kwa kila mbunge, na
kama wabunge wengi wakipinga ina maana Rais atalivunja bunge na hivyo
kufanyika uchaguzi mwingine, kitu ambacho wabunge wa CCM hawatakubali.
Nassari alia na wabunge wa CCM
Katika hatua nyingine, kutokana na
uamuzi huo wa kutolewa nje Mnyika, wabunge kadhaa wa Chadema pia
walitoka kwa hiari yao, akiwapo Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari ambaye alisema wakati anagombea ubunge hakudhani kuwa
bunge kama chombo kikubwa cha uamuzi, chenye umuhimu mkubwa kwa
Watanzania hasa kipindi hiki cha kupitisha bajeti, linaweza kutumiwa
kama mkutano wa chama na kutupiana mipasho.
“Nimesikitika sana nimeona ni bora
nitoke, bunge limekuwa la mlengo wa kisiasa na kupeana mipasho,
nasikitika Mnyika kutolewa nje.
Alisema Mbunge wa Mtera, Livingstone
Lusinde alitoa kauli za kuudhi wapinzani, lakini spika alimwambia arejee
maneno yake mara ya pili,” alisema Nassari.
Kabla ya Mnyika kutolewa nje, Mbunge wa
Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa, pia alionywa na Ndugai
kutokana na kutoa kauli za kumpinga pale alipomtaka Mnyika afute kauli
yake.
“Naomba wananchi wa Iringa mjini,
kupitia Mchungaji Msigwa ni vizuri kuwa na nidhamu kwa bunge hili. Hiki
ni kikao kikubwa, anayezungumza ni Mnyika nimemkataza kuita mtu chizi…,
muache hii habari ya kuropoka kama una jambo simama, kiti ndio kina
uamuzi wa mwisho,” alisema Ndugai.
Pia Ndugai, alikataa mwongozo wa Mbunge
wa Nyamagana, Ezekia Wenje ambaye alitaka mwongozo, kuhusiana na kauli
za kuudhi ambazo zilitolewa juzi na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi.
Nchemba atuzwa Sh210,000
wa Uchumi na Fedha wa CCM, juzi alituzwa
Sh210,000 baada ya kuiponda bajeti ya upinzani na kuiita ni ya kipuuzi
na haitekelezeki, wapinzani wamejaa uigizaji na kumrushia kombora
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa anawahadaa Watanzania
kwa kukataa gari kuukuu, na baada ya ya kupewa jipya alikubali kimya
kimya.
Nchemba akizungumza na waandishi nje ya
bunge, alisema jumla ya fedha alizopewa na wabunge na mawaziri kadhaa
zilifikia Sh210,000.
Mchango wa Lusinde
Mbunge wa Mtera-CCM, Livinstone Lusinde alisema bajeti ya upinzai ya uongo na haitekelezeki.
Lisinde huku akieleza kumuunga mkono,
Nchemba alisema yaliyoandikwa hayana uhusiano na ilani ya uchaguzi wa
Chadema, kwani waliwahi kusema watatoa elimu bure lakini suala hilo
halimo kwenye bajeti.
Kauli hiyo ya Lusinde ilimfanya Naibu
Spika kumtaka airejee tena, naye akarudia maneno yake kuwa hutuba hiyo
ya bajeti kivuli ya upinzani inatofautiana na Ilani ya Uchaguzi ya
Chadema kwani suala la elimu bure halipo.
Lusinde pia alimrushia alisema Mbowe
ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, anajidai kukataa posho
ya Sh80,000 lakini, anakubali malipo ya Sh2 milioni kwa mwezi huku
akitembelea gari la kifahari la Serikali.
No comments:
Post a Comment