



Kampuni ya Vodacom Tanzania leo inafuturisha zaidi ya watoto mia tano kutoka madrasa za mjini na nje ya mji wa Tanga katika viwanja vya Ma-awal Islamic ikiwa ni uzinduzi rasmi wa utaratibu wake wa kila wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan wa kujali na kuonesha upendo kwa watoto yatima na makundi yasiyojiweza kwenye jamii – Ramadhan Care & Share.
Futari hiyo inayoandaliwa na Vodacom kupitia kitengo chake cha misaada kwa jamii – Vodacom Foundation itahudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu na viongozi wa serikali mkoa wa Tanga.
Mapema jana Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mheshimiwa Chiku Gallawa alitoa baraka zake kwenye futari hiyo alipotembelewa ofisini kwake na Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Bw. Salum Mwalim na Meneja Mahusiano kwa Umma Bw. Matina Nkurlu kwa lengo la kusalimiana.
“Utaratibu wa kuwakumbuka yatima ni utaratibu mzuri nawapongeza Vodacom kwa upendo wenu nasikitika sana kwamba sitokuwepo kama nilivyowaeleza wakati mliponitumia ujumbe wa mualiko kwamba nitakuwa safarini Wilayani Handeni kikazi, ila nawatakia kila la kheri na nitawakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mheshimiwa Halima Dendegu”Alisema Mh. Gallawa.
Chini ya utaratibu huo Vodacom Tanzania pia itafuturisha watoto yatima na wa-Madrasa katika miji mbalimbali nchini sanjari na utoaji wa sadaka za vyakula na vifaa vya shule kwa watoto hao.
No comments:
Post a Comment